27 Oktoba 2026 - 17:27
Ayatollah Sayyid Mojtaba Khamenei Asisitiza Kuhifadhi Umoja na Usalama wa Taifa

Ayatollah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, katika mkutano wake na Meja Jenerali Mohsen Rezaei, aliitaja Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na sekretarieti yake kuwa “makutano ya mikakati na mipango” ya masuala ya nchi.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Meja Jenerali Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, amekutana na Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika mkutano huo, Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei alilitaja Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na sekretarieti yake kuwa “makutano ya mikakati na mipango” ya masuala ya nchi. Pia alisisitiza kuwa sekta nne za utamaduni, siasa, uchumi na usalama zinaathiriana, hivyo maamuzi katika kila sekta yanapaswa kuambatana na mipango inayozingatia uhusiano huo.

Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu alieleza kuwa maamuzi madhubuti na yenye msingi imara yanahitaji ramani ya utekelezaji inayozingatia picha kamili ya kila hatua, kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Miongoni mwa mada nyingine zilizojadiliwa katika mkutano huo ni kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa, kujenga uaminifu wa pande zote kati ya wananchi na viongozi, pamoja na kutumia uwezo uliopo katika Katiba, hususan Ibara ya 176, kusaidia Rais na vyombo vya utendaji kurahisisha na kuharakisha utatuzi wa matatizo ya nchi.

Mada nyingine zilikuwa ni kulinda usalama wa kitaifa na kikanda kupitia usimamizi wa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuimarisha uhusiano wa pande mbili na nchi jirani kwa msingi wa maslahi ya kudumu na yenye manufaa kwa pande zote.

Kiongozi huyo alitaja kushindwa kwa adui kufikia malengo yake kuwa miongoni mwa matokeo ya upinzani na ustahimilivu wa kitaifa. Alisisitiza pia umuhimu wa kutoa taarifa kwa umma kwa wakati na kwa juhudi endelevu, ili wananchi waendelee kushiriki katika kuilinda nchi na mfumo wake.

Aidha, alisisitiza kufuatilia upatikanaji wa haki na maslahi ya taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu, pamoja na yale ya Mhimili wa Muqawama (Upinzani), kwa kutekeleza masharti yaliyotangazwa na viongozi wa nchi kwa lengo la kumaliza vita na kuondokana na hali ya “kutokuwa vitani wala kuwa katika amani.”

Katika mkutano huo, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa aliwasilisha ripoti kuhusu hali ya nchi katika sekta mbalimbali na juhudi zinazoendelea kufanyika.

Katika ripoti yake, Dkt. Mohsen Rezaei alieleza kuwa miongoni mwa hatua zinazotekelezwa na sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ni kufuatilia sera ya kimkakati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya “kuweka utaratibu na mfumo wa kikanda unaojitegemea, unaotokana na uwezo wa ndani wa eneo lenyewe.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha